Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

TAASISI YA USULUHISHI WA MALALAMIKO NA TAARIFA ZA KODI

"Haki na Usawa"

TOST YATOA ELIMU KWA WANANCHI KATIKA MAONESHO YA 20 YA BIASHARA AFRIKA MASHARIKI

Imewekwa: 02 Sep, 2025
TOST YATOA ELIMU KWA WANANCHI KATIKA MAONESHO YA 20 YA BIASHARA AFRIKA MASHARIKI

Wananchi wameendelea kupata Elimu juu ya uwepo wa Ofisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST) na namna ofisi hiyo inavyotekeleza majukumu yake katika kuwasaidia Wafanyabiashara na Wananchi kupata msaada wa usuluhishi wa malalamiko ya kodi. Akizungumza na Wananchi hao, Bw. Aderickson Njunwa ambaye ni Afisa sheria mkuu katika ofisi ya TOST amewaeleza wananchi kuwa ofisi hiyo imeanzishwa na serikali kwa lengo la kushughulikia Taarifa na kutatua malalamiko ya kodi kwa njia mbadala ili kuboresha ukusanywaji wa mapato kwa kupunguza au kuondoa malalamiko katika mfumo wa usimamizi wa kodi.

Elimu hiyo inaendelea kutolewa kwa Wananchi na Wafanyabiashara katika kanda ya Ziwa na mikoa jirani wanaotembelea Banda la TOST lililopo katika Maonesho ya 20 ya Biashara Afrika Mashariki yanayofanyika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza. Wananchi hao wamekiri kuwa uwepo wa ofisi hiyo utaongeza ulipaji kodi na kuchochea ari ya Wafanyabiashara na Wananchi kulipa kodi kwa hiari.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Huduma za Taasisi Bw. David Alal amewaeleza Wananchi hao kuwa wanaendelea kupeleka Elimu hiyo mikoa mbalimbali kuhusu majukumu ya ofisi hiyo pamoja na kushiriki matukio mbalimbali ya utoaji Elimu kwa umma ikiwemo maonesho kwa ajili ya kuendelea kujitambulisha kwa Wafanyabiashara na Wananchi kwa ujumla.