Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

TAASISI YA USULUHISHI WA MALALAMIKO NA TAARIFA ZA KODI

"Haki na Usawa"

NAMANGA NI LANGO LA UCHUMI NA USHIRIKIANO

Imewekwa: 17 Sep, 2025
NAMANGA NI LANGO LA UCHUMI NA USHIRIKIANO

Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi Bw. Erastus Mtui amesema mpaka wa Namanga uliopo Arusha, unaoziunganisha nchi za Kenya na Tanzania ni lango la uchumi na ushirikiano wa Nchi za Afrika mashariki kwasababu mpaka huo ni eneo muhimu la kukuza biashara na ushirikiano baina ya Nchi hizo.


Bwana Mtui ameeleza hayo Septemba 15, 2025 alipofanya ziara ya Mpango wa ushirikishwaji na uhamasishaji wa wadau wa mpakani kuhusu uwepo wa Ofisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi, Msuluhishi amewapongeza watendaji wa mpaka huo uliyopo wilayani Longido Mkoani Arusha kwa namna wanavyotekeleza wajibu wao kwa manufaa ya mataifa ya Tanzania na Kenya bila kusahau mataifa mengine yanayotegemea bidhaa mbalimbali zinazopita mpakani hapo.


Akiwa ameambatana na maafisa wenzake, Msuluhishi amesema lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kujifunza na kuona namna gani kazi za kila siku zinatekelezwa mpakani hapo pamoja na kuitambulisha ofisi ya usuluhishi wa malalamiko na Taarifa za kodi kwa wadau wa mipakani.