Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

TAASISI YA USULUHISHI WA MALALAMIKO NA TAARIFA ZA KODI

"Haki na Usawa"

KUTATUA NA KUSULUHISHA MIGOGORO YA KODI NI JUKUMU LETU.

Imewekwa: 07 Jun, 2024
KUTATUA NA KUSULUHISHA MIGOGORO YA KODI NI JUKUMU LETU.

Ofisi ya Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi imekasimiwa kisheria jukumu mahususi la kupokea na kusuluhisha malalamiko ya kodi kutoka kwa Wananchi ambayo inatokana na usimamizi wa sheria za kodi zinazosimamiwa na mamlaka ya mapato nchini.

Ofisi hii ni yenu wananchi wala msiiogope ipo kwa mujibu wa sheria na imeanza kazi rasmi kutekeleza Januari 23, 2024 mahususi kwa ajili ya kupokea Malalamiko na Taarifa za kodi kwa lengo la kutatua na kusuluhisha migogoro ya kodi kwa njia ya Usuluhishi na Upatanishi, huduma hiyo iantolewa bila kulipia gharama yoyote kwa Msuluhishi, inatolewa kwa njia  rahisi zaidi kuliko njia za kimahaka.

Juhudi zote hizi zimefanywa na Serikali ili kuwaondolea wananchi Kero katika swala zima linalohusiana na Kodi lakini pia kuwakumbusha wananchi majukumu na wajibu wao wa kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa letu. Hii inamaanisha kuimarisha na kusimamia mfumo mzima wa ukusanywaji wa kodi nchini.

Kaimu Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi Bw. Godwin Barongo aliyasema hayo alipokuwa akiwasilisha historia fupi ya uwepo wa Ofisi hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Elimu kwa Umma katika  jiji la Dodoma yenye nia na dhimira ya kuhabarisha umma juu ya shughuli zinazofanywa na ofisi hii katika kutatua na kusuluhisha migogoro ya kodi na kauli mbiu yake ni kataa ukwepaji wa kodi na kata kodi za dhuluma.

Kauli mbiu hii inalenga kusisitiza wajibu wa kila mmoja wetu juu ya haki, usawa na wajibu katika ulipaji na ukusanywaji wa kodi mujibu wa sheria zilizopo kama alivyosisitiza Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DKT. SAMIA SULUHU HASSAN wakati akiingia madarakani na hata alipotimiza miaka mitatu ya kuwa madarakani alirudia tena kusisitiza na kuhimiza watanzania kukataa ukwepaji wa kodi na kukataa kodi za dhuluma.