BANDA LA TOST SABASABA NI KITOVU CHA USULUHISHI WA MALALAMIKO YA KODI
Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) ametoa rai kwa Wananchi na Wafanyabiashara kutembelea Banda la Ofisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (@tostanzania ) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwl. J.K. Nyerere, ili kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na ofisi hiyo.
Rai hiyo imetolewa leo tarehe 2 Julai, alipotembelea Banda la TOST lililopo ndani ya Jengo la Wizara ya Fedha na kuhimiza Wananchi na Wafanyabiashara kutembelea banda hilo ili waweze kupata elimu kuhusu majukumu ya TOST, pamoja kupewa suluhisho ya malalamiko na taarifa zao za kodi.
Balozi Omar amesema kuwa huduma zinatolewa na TOST zinachangia kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato, kuboresha mazingira ya biashara na kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi, Bw. Erastus Mtui, amesema TOST imeweka kambi katika maonesho hayo ili kutoa elimu kwa wananchi na wafanyabiashara sambamba na kupokea
malalamiko na taarifa za kodi kutoka kwa wananchi pamoja na kuzifanyia kazi kwa wakati kwa mujibu wa sheria ili kuongeza wigo wa ukusanywaji wa Kodi pamoja na ulipaji kodi wa hiari.